Release No. 188
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 28, 2012
KILIMANJARO STARS YAPOTEZA MECHI YA CHALENJI
Tanzania
Bara (Kilimanjaro Stars) imepoteza mechi ya michuano ya Kombe la
Chalenji baada ya kufungwa bao 1-0 na Burundi katika mchezo uliofanyika
leo (Novemba 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Mandela ulioko Namboole
jijini Kampala, Uganda.
Bao
hilo lilifungwa na Seleman Ndikumana dakika ya 52 kwa penalti. Mwamuzi
Ronnie Kalema wa Uganda aliamuru adhabu hiyo baada ya Shomari Kapombe
kumwangusha mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba.
Washambuliaji
wa Kilimanjaro Stars walilishambulia lango la Burundi kwa muda mwingi
wa mchezo wakitafuta bao la kusawazisha. Hata hivyo mashuti ya John
Bocco, Mrisho Ngasa na Amri Kiemba aliyeingia badala ya Simon Msuva ama
yalitoka nje au kuokolewa na kipa Arthur Arakaza.
Akizungumza
mara baada ya mechi hiyo, Kocha wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen
amesema ilikuwa ngumu hasa kutokana na uwanja kuwa na matope
yaliyotokana na mvua iliyonyesha saa chache kabla ya kuanza mchezo huo
wa kundi B.
“Katika
hali ile ya uwanja ukifanya kosa ni ngumu kulifuta. Tuliruhusu penalti.
Tulitengeneza nafasi nyingi, lakini kipa wa Burundi alikuwa kikwazo
kikubwa kwetu. Katika mpira wa miguu ukishindwa kufunga unapoteza
mchezo,” amesema Kim ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuiongoza
Kilimanjaro Stars kwenye michuano ya Chalenji.
Kilimanjaro
Stars yenye pointi tatu baada ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Sudan
katika mechi yake ya kwanza, itamaliza mechi za hatua ya makundi Desemba
Mosi mwaka huu kwa kucheza na Somalia.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment