|
Wachimbaji Madini Wadogo katika shughuli ya uokozi |
Imebainishwa kuwa vifo
vinavyotokea kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa
Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara vinatokana na uzembe katika
uchimbaji wa baadhi ya migodi hiyo.
Hayo
yamebainishwa na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini
Mhandisi Benjamin Mchwampaka kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo mameneja
wa migodi yaliyofanyika ukumbi wa Kazamoyo Inn mjini Mirerani mkoani
manyara..
Aidha aliongeza kuwa
tangu mwezi Januari hadi Mei mwaka huu wachimbaji wadogo 11 wamepoteza
maisha kwenye machimbo ya migodi ya Tanzanite katika matukio tofauti.
“Matukio
hayo ni vifo sita vya kuangukiwa na dunganya,vifo viwili kwa kukosa
hewa au kuvuta hewa chafu migodini na kuteleza kwenye ngazi,kulipuliwa
na baruti na kuangukiwa na mwamba kifo kimoja,” alisisitiza Mchwampaka.
Alikemea
vikali tabia ya baadhi ya wachimbaji wadogo kutumia baruti kama silaha
badala ya kuzitumia kwa nyenzo za kazi kwa kuzifanya mabomu ya kienyeji
na kuwalipua wachimbaji wenye migodi yenye uzalishaji.
“Serikali
haitavumilia tena vitendo hivi na wote watakaohusika na jambo hilo
mgodi wao utafungwa mara moja na tutafuta leseni zao kabla ya
kuwachukulia hatua nyingine za kisheria,” alisema Mchwampaka.
Naye
mwenyekiti wa Chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema)
Zephania Mungaya aliishukuru Serikali kutoa mafunzo hayo ambayo
yatawanufaisha wachimbaji wadogo kupitia mameneja hao wa migodi.
“Napenda
kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali kwa kuandaa mafunzo haya
ambayo yatazidi kuwajengea uwezo mameneja wa migodi ambao ndiyo daraja
baina ya wamiliki wa migodi,wachimbaji na Serikali,” alisema Mughaya.
Kwa upande wake Ofisa madini mkazi wa Mirerani Laurent Mayala alibainisha kuwa lengo
la mafunzo hayo ni kupunguza ajali migodini kwa kuwaongezea mbinu na
elimu ya usalama na sheria ya madini ili kuboresha hali ya uchimbaji
salama migodini.
Alimalizia kusema kuwa mada
zitakazotolewa ni usalama migodini,uzoefu na changamoto,sera na sheria
ya madini,upelekwaji hewa migodini,matumizi ya baruti na tahadhari
zake,wajibu na majukumu ya meneja na jiolojia ya miamba ya
Tanzanite.
|
No comments:
Post a Comment