Monday, October 24, 2011

WANANCHI IGURUSI: KITUO CHA AFYA WANATUONEA KWA NINI TULIPIE HUDUMA YA AMBULANCE?

MBARALI, 24/10/2011

WANANCHI wanaoishi katika mji mdogo wa igurusi wilayani Mbarali Mkoani Mbeya wameulalamikia uongozi wa kituo cha afya katika mji huo kwa kuwatoza gharama za kuwasafirisha wagonjwa wanaohitaji msaada wa kukimbizwa katika hospitali ya jirani na gari la kubebea wagonjwa la kituo pindi wanapokuwa wamezidiwa.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama cha Demokrasia na Maendeleo,CHADEMA wananchi hao wamesema kuwa wamekuwa wakitozwa pesa ili wapatiwe msaada wa kupelekwa hospitali nyingine kwa matibabu zaidi pindi inapokuwa imeshindikana kutibiwa katika kituo hicho.

wamesema wamekuwa wakitozwa pesa kiasi cha shilingi 35,000 hadi 45,000 ili wagonjwa wao wapelekwe katika hospitali ya Chimala ambapo pana urefu wa Kimometa 15 toka Igurusi hali ambayo kwa wastani gari inatumia lita mbili.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Kituo hicho ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Dr.Sichalwe alipohojiwa na Ushindi Redio kwa njia ya simu amesema yeye hana taarifa na malalamiko hayo na kusema kuwa si msemaji wa mambo hayo na kusema kuwa msemaji ni mganga mkuu wa wilaya.

Naye Diwani wa kata hiyo ya Igurusi Kenneth Ndingo amekiri kuwepo kwa tatizo la mafuta kwa gari hilo na kusema kuwa wananchi walikwisha elezwa juu ya uchangiaji wa mafuta katika gari hilo kwa kuwa lililetwa gari bila kuwepo kwa bajeti ya mafuta.

Aliongeza kuwa kuhusu gari hilo la wagonjwa kufanya shughuli za kituo cha polisi ni kweli kwa kuzingatia umuhimu wa kazi yao,lakini pia kuhusiana na kubeba baadhi ya watu kuwapeleka katika maeneo ilipo minada alisema hana taarifa huku akisema kuwa ikumbukwe gari hilo liko chini ya mganga mkuu wa kituo hicho hivyo asingeweza kujua kila kitu kinachofanywa na gari ilo.

No comments:

Post a Comment