Sunday, December 2, 2012

WITO UMETOLEWA KWA WANACHAMA WA CHADEMA KUTOWAOGOPA CCM NA JESHI LA POLISI

Chato

VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),wametakiwa kuwajengea uwezo wa ujasiri wanachama wao ili kuondokana na uoga wa kuwaogopa wanachama wa CCM ama jeshi la polisi.

Profesa Kulikoyela Kahigi (Mb)
Wito huo umetolewa na mbunge wa Bukombe, Profesa Kulikoyela Kahigi (Chadema) alipokuwa akizungumza na viongozi wa  chama hicho ambao wapo Wilaya ya Chato Mkoani Geita kutokana na malalamiko waliyotoa kwa mbunge huyo kwa madai kuwa viongozi wengi na wanachama wa Chadema wanatishiwa na baadhi ya viongozi wa CCM pamoja na baadhi ya asikari wa jeshi la polisi.

Wananchama hao wamesema kuwa licha ya kujitahidi kujenga chama,lakini bado wananchama pamoja na viongozi wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa na kuonewa na baadhi ya viongozi wa CCM pamoja na jeshi la wananchi.


“Mbunge tunataka tukueleze wazi kuwa huku tunafanya kazi katika mazingira magumu, hapa anapoonekana mtu ambaye ni mwelewa wa mambo mbalimbali na kuhoji mambo ya kimaendeleo anabambikiwa kesi na wakati mwingine kutishiwa kupelekwa polisi…

“Mbali na kubambikiwa kesi pia viongozi wa CCM wamekuwa wakiwatishia wananchi kwa madai kuwa vyama vya upinzani vipo kwa ajili ya kuleta fujo hivyo kuwafanya wananchi wengi kuogopa kujiunga na vyama hivyo hususani Chadema” walisema viongozi hao.

Kwa upande wake Profesa amewataka viongozi kusimama kidete kuhakikisha wanatoa elimu kwa raia na kuwaeleza kuwa vyama vingi havikusajiriwa kwa ajili ya kuleta fujo.
Ramani inayoonyesha wilaya ya Chato

Amesema kama vyama vya upinzani vingekuwa na lengo la kuleta fujo nchini ni wazi kuwa visingeweza kusajiliwa na kuwakumbusha kuwa chama kinachoweza kuleta fujo mahali pote nchini ni chama tawala kwani ndicho chenye dola.

“Ngoja niwaambie ndugu zangu hao maaskari wanaowatishia wao kama nani waambieni kuwa nyinyi mnakaa nao mitaani na kila siku mnakutana nao Jeshi la polisi linatakiwa kuhakikisha kulinda usalama na mali ya raia lakini siyo kufanya kazi ya siasa” alisema Profesa.

Wakati huo huo amewataka watanzania kote nchini kutowachagua viongozi ambao wanatumia fedha zao nyingi kwa ajili ya kuwashawishi wananchi wawachague katika nafasi mbalimbali ambazo ni za kuchaguliwa.
Baadhi ya wananchi wilayani Chato wakikabidhi kadi za chama cha Mapinduzi baada ya  CHADEMA kufanya mkutano wa siasa mapema mwezi Julai mwaka huu.(PICHA KWA HISANI YA CHADEMA)

Profesa Kahigi ametoa rai hiyo wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Seventh Day Adventist, lililopo Wilayani Chato Mkoani Geita Kata ya Mganza tarafa ya Nyamilembe.

Mbunge huyo amesema kuwa wapo baadhi ya viongozi ambao hawana hofu ya kimungu na hao wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuwashawishi wananchi kuwachagua inapofikia nyakati za chaguzi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment