Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini-TFF Boniface Wambura |
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) chini ya uenyekiti wa Alex Mgongolwa ilikutana Desemba 30 mwaka
jana kupitia masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake ikiwemo taarifa ya uamuzi wa timu ya Kimbangulile kukata rufani Kamati ya Rufani kupinga uamuzi wake juu ya mchezaji Mbwana Samata.
Ikumbukwe kuwa Kimbangulile iliwasilisha malalamiko TFF ikieleza kuwa inastahili
malipo baada ya Simba kumuuza Samata kwa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Kimbangulile ilitaka ilipwe fidia ya mazoezi (training compensation) na mchango
maalumu (solidarity contribution) kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji
za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Uamuzi wa Kamati ya Mgongolwa ulikuwa Kimbangulile imeshindwa kutoa vielelezo
kuonesha kuwa iliingia gharama za mazoezi kwa mchezaji husika wakati akiichezea
timu hiyo.
Kwa upande wa solidarity contribution ambayo ni asilimia 5 ya mauzo ya mchezaji
huyo TP Mazembe, fedha hizo zinatakiwa kulipwa na klabu yake hiyo mpya ambayo
TFF itaitaka kufanya hivyo wakati Samata atakapoombewa Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC).
Hivyo Kamati itatengeneza utetezi wake na kuuwasilisha kwenye Kamati ya Rufani itakaposikiliza rufani ya Kimbangulile.
USAJILI WA DIRISHA DOGO 2011/2012
Kwa upande wa Daraja la Kwanza, Kamati hiyo imetoa siku saba kwa klabu ambazo
zimezidisha idadi ya wachezaji ili zipunguze, kwani kila timu inatakiwa kuwa na
wachezaji wasiozidi 30.
Klabu nyingi baada ya kufanya usajili wa dirisha dogo zimepitisha idadi ya
wachezaji 30 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni.
Hivyo kwa klabu ambayo itashindwa kupunguza wachezaji ndani ya muda huo, TFF itahesabu hadi 30 na wachezaji watakaokuwa wamezidi wataondolewa.
Kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), klabu ya Villa Squad ndiyo imekutwa na
kasoro katika usajili wake ambapo imetoa kwa mkopo wachezaji wanne na imepokea
wengine watano kwa mkopo.
Kwa mujibu wa kanuni ya mkopo, klabu haitakiwi kuwa na wachezaji zaidi ya watano
iliotoa au kuingiza kwa mkopo kwa wakati mmoja. Hivyo Villa Squad imetakiwa
kuwaandikia barua za kuwaacha wachezaji wanne iliowatoa kwa mkopo ili wawe huru
(free agents).
Pia Kamati imeagiza viongozi wa juu wa Majeshi ambayo yanamiliki timu za mpira
wa miguu kupewa elimu ya kanuni za usajili, kwani mafunzo ya kijeshi na uhamisho
wa wachezaji ambao ni askari vimekuwa vikiathiri viwango vya timu zao kwenye
ligi.
SIMBA KUMSIMAMISHA KOCHA BASENA
Malalamiko ya Kocha Moses Basena kwa TFF baada ya klabu yake ya Simba
kusimamisha mkataba wake yaliwasilishwa mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na
Hadhi za Wachezaji.
Baada ya kupitia malalamiko hayo, uamuzi wa kamati ni kuwa suala hilo liendelee
kuwa kati ya Simba na Basena na kuwataka wakae pamoja ili waweze kulipatia
ufumbuzi.
Licha ya Basena kuwa na mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, Kamati imebaini
kuwa hauwezi kufanya kazi (functional) kwa vile kocha huyo hakuwa na kibali cha
kufanya kazi nchini (work permit).
Hivyo kisheria hakukuwa na mkataba kwa vile ili Basena aweze kuitumikia Simba ni
lazima awe na kibali cha kufanya kazi nchini.
TFF ilikataa maombi ya Simba kuiandikia barua Idara ya Uhamiaji kuthibitisha barua ya kumuombea work permit baada ya kocha huyo kushindwa kuwasilisha vyeti vyake vya ukocha.
Kwa vile Simba imeshaajiri kocha mwingine (Milovan) kwa mkataba wa miezi sita na
kupatiwa kibali cha kufanya kazi nchini, ufumbuzi wa suala la Basena unabaki
kuwa kati ya klabu hiyo na kocha huyo.
Imetolewa na: Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
No comments:
Post a Comment