Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Rais Jakaya Mrisho Kikwete |
”Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Athumani Mhina, aliyekuwa kiongozi shupavu na mwadilifu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake.
Rais Kikwete amesema: “Nilimjua Mheshimiwa Mhina enzi za uhai wake. Katika nafasi zote alizozishikilia katika utumishi wa umma, Marehemu Mhina alitoa mchango mkubwa ikiwa ni pamoja na kufanya jitihada kubwa na nyingi kuimarisha Jumuiya ya Wazazi. Hivyo kifo chake ni pigo kubwa siyo tu kwa Jumuiya hiyo bali pia kwa Chama chetu cha Mapinduzi na kwa wana-CCM kwa ujumla kote nchini. Kifo hiki kimeacha pengo ambalo si rahisi kuzibika.”
Rais Kikwete amemuomba Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama kumfikishia salamu zake za pole kwa familia ya marehemu Athumani Mhina. “Natoa pole nyingi na za dhati kabisa kwa familia ya Marehemu kwa kupoteza mhimili madhubuti wa familia. Namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ailaze mahali pema peponi roho ya Marehemu Athumani Mhina, Amina”, amesisitiza Rais Kikwete katika salamu zake.
Rais Kikwete ameihakikishia familia ya Marehemu kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huo mkubwa, na amewaomba wanafamilia na ndugu wengine kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza kifo cha mpendwa wao kwani yote ni mapenzi yake Mola.
No comments:
Post a Comment