Na:Mwandishi Wetu,Manyara
Mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Ally Dengu (26) wa kijiji cha Bonga wilayani Babati Mkoani Manyara amefariki dunia baada ya mtumbwi aliokuwa akiendesha kupinduliwa na mnyama Kiboko akiwa katika shughuli za uvuvi katika Ziwa Babati.
Mnyama Kiboko |
Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara Lebaratus Sabas amedhibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tukio hilo limetokea siku ya tarehe 1 Januari mwaka huu majira ya saa 11 jioni ambapo marehemu alikuwa katika shughuli zake za uvuvi.
Amewataka wavuvi wa ziwa hilo kuwa makini wakati wanapokuwa katika shughuli zao za uvuvi hata kama wanyama hao wamezoeana nao kwani huwezi kujua lini mnyama anabadilika kwa mfano kiboko anapokuwa amezaa huwa mkali.
Kwa upande wake mwenyekiti za wavuvi wa ziwa hilo Idd Hassan akiongea na Mwandishi wa Blog hii Mkoani Manyara wavuvi hao wameiomba serikali kuwasaidia ili kuweza kuwapunguza viboko hao kwani viboko hao wanaendelea kusababisha adha kubwa kwa wavuvi pamoja na wakulima wanaolima kando kando ya ziwa hilo.
Ameongeza kuwa forodha hiyo ya mbalakuu ndio kubwa kuliko zote katika ziwa Babati na ndio tegemeo la usambazaji wa samaki ndani ya mji wa Babati na nje ya mji huo hivyo Halmashauri inapaswa kuwajali wavuvi wa eneo hilo kwa kuwahakikishia usalama wa kutosha
Wakati huo huo Issa Saidi ambaye pia ni mvuvi na shuhuda wa tukio hilo amesema kuwa ilikuwa majira ya saa 11 za jioni wakiwa Ziwani walimwona marehemu akishambuliwa na kiboko na kwamba alipiga kelele za kuomba msaada lakini kwa kuwa mnyama huyo alikuwa karibu na marehemu wao walishindwa kumsaidia.
Takwimu zinabainisha kuwa Katika mwaka 2011 pekee wamekufa watu wanne kutokana na kuuwawa na viboko ambao wamekuwa wakiwashambulia wavuvi wakiwa katika shughuli zao za uvuvi ambapo wavuvi hao walishapeleka malalamiko yao kwa viongozi wahusika lakini mpaka sasa hakuna kiboko aliyeuwawa au kudhibitiwa.
No comments:
Post a Comment