Na Mohammed
Mhina wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
ZANZIBAR NOVEMBA 15, 2013. Jeshi la
Polisi Zanzibar limewakamata watuhumiwa wemhine watatu wakiwemo Maafisa wawili
wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA kituo cha Bandari Zanzibar kwa kuhusika na kashfa
ya kupatikana kwa meno ya tembo yenye thamani ya Mabilioni ya shilingi.
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP
Mussa Ali Mussa, amewataja Maafisa hao wa TRA waliokamatwa kuwa ni Omari Hamad
Ali(50) na Mohammed Hija(48) ambao wote wanafanyia kazi katika Bandari ya
Zanzibar. Mtuhumiwa mwingine ni kibarua wa Mamlaka ya bandari Zanzibar Haidar
Ahmad Abdallah(54).
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao
kunaifanya idadi ya watuhumiwa waliokamatwa hadi sasa kwa kuhusika na sakata
hilo kufikia watano.
Kamishna Mussa amesema Watuhumiwa
wengine wawili ambao ni wafanyakazi wa Kampuni ya Uwakala wa Mizigo ya Island
Sea Food Limited, Mohammed Suleiman Mussa(45) na Juma Ali Makame(34) wao walikamatwa
siku ya tukio la kukamatwa kwa meno hayo ya tembo kwenye Bandari ya Zanzibar.
Tayari watuhumiwa hao wamesafirishwa
kwenda Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Pamoja na mambo mengine, kusafirishwa kwa watuhumiwa hao kwenda Jijini
Dar es Salaam, kunatokana na Zanzibar kutokuwa na Sheria maalumu
inayohusu wanyamapori.
Maafisa wa Idara ya Wanyamapori
nchini, leo wamekamilisha kazi ya kuhesabu na kulinganisha vipande 1,023 vya
meno ya tembo vilivyokamatwa jana kwenye Bandari ya Zanzibar na kubaini idadi
ya tembo waliouawa kuwa ni 305.
Meno hao yenye uzito wa kilo
2,915 yenye thamani ya Dolla 4,775,000
sawa na shilingi 7,480,125,000 za Tanzania (Bil.7.4), yalikamatwa juzi yakiwa
yamehifadhiwa katika magunia 98 na kuwekwa kwenye konteina moja la futi 40
lenye namba PCIU 857619/0 lillilokuwa tayari kupakiwa kwenye meli ya MV Kota
Henning kupelekwa nchini Ufilipino kwa magendo.
Hadi sasa bado Makachero wa Polisi
wa Kimataifa Interpol hapa nchini kwa kushirikiana na Makachero wa Polisi
Zanzibar, idara ya wanyamapori makao makuu wanaendelea na upelelezi wa
kuwabaini wale tote waliohusika na kashfa hiyo.
Jana Kamishna wa Polisi Zanzibar CP
Mussa Ali Mussa, alisema kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kuhakikisha kuwa upelelezi
wa kina unafanyika ili kuwakamata wale wote wanaohusika na mtandao huo.
Alisema hadi sasa Jeshi la Polisi
bado linamsaka tajiri aliyewezesha mipango ya kukusanywa na kusafirisha shehena
hiyo kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar ili kusafirishwa nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment