Wednesday, January 16, 2013

PRECISION AIR YAZINDUA SAFARI ZA ANGA DAR-MBEYA


Ndege ya  Precion Air ikitua katika uwanja wa Songwe.PICHA:MBEYA YETU
Na: Kamuli Tete wa Habarika

Shirika binafsi la ndege hapa nchini la Precion Air leo Jan 16 ,2013 limezindua rasmi safari zake kati ya Dar es Salaam na Mbeya.

 Shughuli hizo za Uzinduzi zimefanyika katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe uliopo nje kidogo ya jiji la Mbeya

 Akizungumza katika uzinduzi wa safari za ndege za shirika hilo kati ya Dar es salaam na Mbeya Mwenyekiti wa shirika hilo ndugu Michael Shirima amesema Shirika hilo limedhamiria kutoa huduma za usafirishaji wa abiria zenye ubora 

Ndugu Michael Shirima Mwenyekiti Precion Air
Kuzinduliwa kwa ruti ya Mbeya, kutalifanya shirika hilo kuwa na jumla ya ruti 16, na shirika hili limepanga kufanya safari hizi mara nne kwa wiki katika ruti hii ambayo ina umbali wa takriban kilomita 680, huku ikitarajiwa kuwa ndege yao mpya iliyozinduliwa hivi karibuni ya ATR 42-600, itatumika kwa safari hizo.

 Hata hivyo Mwenyekiti wa Shirika hilo Michael Shirima amesema changamoto iliyosalia ni ukosefu wa baadhi ya vifaa muhimu vinavyoweza kumsaidia rubani wakati akitua katika uwanja wa Songwe, pia amesema Mamlaka ya Hali ya hewa bado ina changamoto ya kutoa taarifa kwa Marubani ili kuhakikisha ndege ambazo zingepaswa kutua hazirudi Dar es salaam kutokana na hali mbaya ya hewa hususani kuwepo kwa wingu zito.  

 Katika shughuli hizo za uzinduzi wamehudhuria viongozi mbalimbali wa serikali,wafanyabiashara wakubwa jijini Mbeya,wadau wa usafiri wa anga wakiwemo kutoka Mamlaka ya Usafiri wa anga TCCIA,Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA,Waandishi wa Habari na wananchi wa kijiji cha Ikumbi wanaoishi jirani na uwanja huo wa ndege.

Serikali Mkoani Mbeya imewakilishwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dk. Norman Sighala.
Uzinduzi rasmi katika uwanja wa Songwe.PICHA NA MBEYA YETU


Katika hotuba yake Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe amewashauri wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuitumia fursa hiyo ya kuwepo kwa huduma za haraka za usafiri wa anga kutoka kwa shirika hilo 

"Hivyo, ushauri wangu  kwa wakazi wa Mbeya na maeneo ya jirani ni kuanza kutumia fursa iliyoletwa na Kampuni ya Ndege ya Precision Air na Makampuni mengine yatakayokuja hapa Mbeya kuchangamkia biashara.amesema Waziri Mwakyembe 

 Waziri Mwakyembe amesema Kuwepo kwa huduma za usafiri kati ya Dar es salaam na Mbeya kutaongeza shughuli za kiutalii na fursa nyingine za biashara katika mkoa wa Mbeya na mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini.

Mara baada ya Uzinduzi huo ndege hiyo yenye namba 5H-PWG imepaa kurejea jijini Dar es salaam
Precion Air ikiwa angani



No comments:

Post a Comment