Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeitaka klabu ya Yanga kuwasilisha
maelezo ya ziada na vielelezo kuthibitisha hoja zao dhidi ya mwalimu wa zamani
wa klabu hiyo, Kostadin Papic ambaye ameishtaki klabu hiyo akidai malimbikizo
ya mshahara yanayofikia Dola 12,000 za Kimarekani ifikapo Desemba 11, 2012.
Katibu mkuu wa TFF Angetile Osiah amekiri kupokea
barua hiyo kutoka FIFA.
Kostadin Papic, aliyekuwa Kocha wa Yanga |
Yanga, ambayo ilimuondoa kocha huyo Mserbia mwishoni
mwa msimu wa mwaka 2011/12, inadai kuwa ilishafanya malipo kadhaa, yakiwemo
ziada ya gharama za hoteli aliyokuwa akiishi, na kwamba hadi sasa kocha huyo
anadai si zaidi ya Dola 4,000 za Kimarekani ambazo klabu hiyo imesema itamlipa
mara atakapowasilisha ripoti ya ufundi ya kipindi alichokuwa kocha mkuu.
Katika barua yake kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), FIFA imeitaka Yanga kuwasilisha vielelezo hivyo kabla ya
Desemba 11, 2012 baada ya Papic kuliandikia Shirikisho hilo akidai kuwa “haamini
kwamba klabu hiyo itatekeleza ahadi yake ya kulipa deni walilolikubali” na
kutaka kujua itachukua muda gani kulipa baada ya mtaalamu huyo kutoka Serbia
kuwasilisha ripoti yake ya kiufundi kama alivyotakiwa na uongozi wa Yanga.
Katika barua hiyo ambayo imetakiwa iwasilishwe
kwenye uongozi wa Yanga, FIFA imeeleza kuwa kama Yanga haitawasilisha hoja
zaidi na vielelezo ifikapo tarehe hiyo, Shirikisho hilo litachukulia kuwa klabu
haina haja ya kuwasilisha hoja zaidi na hivyo kuendelea na taratibu za kuliwasilisha
suala hilo kwenye Kamati ya Hadhi za Wachezaji kwa ajili ya hatua zaidi na
uamuzi ufanywe kwa mujibu wa nyaraka zilizopo.
Katibu Mkuu wa TFF Angetile Osiah |
Akizungumzia suala hilo, katibu mkuu wa TFF,
Angetilke Osiah alisema barua hiyo ya FIFA itawasilishwa mapema Yanga ili iweze
kujua hatua za kuchukua kuondoa uwezekanbo wa klabu hiyo kuchukuliwa hatua
ambazo zinaweza kuzuilika.
Yanga pia ilikuwa kwenye hatari ya kushushwa daraja
baada ya kushindwa kuwasilisha vielelezo mapema katika sakata lililomuhusu
mchezaji wake wa zamani, John Njoroge ambaye aliishtaki klabu hiyo FIFA akidai
fidia ya takmriban Sh milioni 17 kutokana na Yanga kuvunja mkataba wake bila ya
kufuata taratibu.
Baada ya kuwasilisha mashtaka yake FIFA, Yanga
iliandikiwa barua iwasilishe utetezi wake lakini ikashindwa kufanya hivyo na
kesi hiyo kusikilizwa upande mmoja na Kitengo cha Usuluhishi cha FIFA (DRC) na
kutoa uamuzi ambao ulimnufaisha beki huyo wa Kenya. Katikati ya mwaka, FIFA
ilitoa agizo la kukazia hukumu hiyo ikitoa siku 30 kwa Yanga kumlipa Njoroge na
kwamba ingeshindwa kufanya hivyo suala hilo lingewasilishwa Kamati ya Nidhamu
kwa ajili ya kuchukua hatua.
Katika barua yake, FIFA ilitaja baadhi ya hatua hizo
kuwa ni kupokonywa pointi, kushushwa daraja au kulipishwa faini kubwa.
No comments:
Post a Comment