Na: Boniface Wambura_TFF
LUHENDE AONGEZWA KIKOSINI TAIFA STARS
Beki
wa Yanga, David Luhende ameongezwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa
ajili ya mechi dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) zitakazofanyika
mwakani nchini Afrika Kusini.
Kocha
Kim Poulsen amesema kutokana na uamuzi huo wa kumuongeza beki huyo wa
kushoto amemuondoa mchezaji mmoja kwenye kikosi chake. Mchezaji huyo ni
mshambuliaji Zahoro Pazi wa JKT Ruvu.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager sasa itaingia kambini
kwenye hoteli ya Tansoma jijini Dar es Salaam, Julai 3 mwaka huu badala
ya Julai 4 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Mechi
ya Uganda itachezwa Julai 13 mwaka huu, saa 9 kamili alasiri kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati ile ya marudiano itachezwa wiki
mbili baadaye jijini Kampala, Uganda.
Wachezaji
wanaotakiwa kambini ni Aggrey Morris (Azam), Aishi Manula (Azam), Ally
Mustafa (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo
(Yanga), Haruni Chanongo (Simba), John Bocco (Azam), Juma Kaseja
(Simba), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar) na Kelvin Yondani (Yanga).
Wengine
ni Khamis Mcha (Azam), Mrisho Ngasa (Simba), Mudathiri Yahya (Azam),
Mwadini Ali (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Salum
Abubakar (Azam), Shomari Kapombe (Simba), Simon Msuva (Yanga) na
Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).
TIMU NNE KUCHEZA NUSU FAINALI RCL
Timu
nne zimefuzu kucheza hatua ya nne (nusu fainali) ya Ligi ya Mabingwa wa
Mikoa (RCL) baada ya kushinda mechi zao za hatua ya tatu ya michuano
hiyo itakayotoa washindi watatu watakaocheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL)
msimu ujao.
Katika
hatua hiyo Polisi Jamii ya Mara itaikaribisha Kimondo SC ya Mbeya
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma wakati Stand United
FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Friends Rangers ya Dar es Salaam kwenye
Uwanja wa Azam Chamazi.
Mechi
za kwanza zitachezwa Juni 23 mwaka huu wakati zile za marudiano
zitafanyika kwenye viwanja vya Sokoine jijini Mbeya na Kambarage mjini
Shinyanga, Juni 30 mwaka huu.
Kwenye
hatua ya tatu ya RCL, Friends Rangers iliing’oa Kariakoo ya Lindi kwa
jumla ya mabao 2-0, Stand United FC ikaitoa Machava FC ya Kilimanjaro
kwa mabao 2-1, Kimondo SC ikaishinda Njombe Mji mabao 6-5 wakati Polisi
Jamii iliitambia Katavi Warriors kwa mabao 7-6.
Hatua
ya mwisho ya ligi hiyo itachezwa Julai 3 mwaka huu kwa mechi za kwanza
wakati zile za marudiano zitakuwa Julai 7 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment