Sunday, January 20, 2013

MICHEZO:Licha ya 'kubafuliwa' na Leopards Stewart Hall Asema Timu yake Ilicheza Vizuri

NAIROBI

Licha ya kupoteza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya A.F.C Leopard, kocha wa Azam FC Stewart Hall amesema timu yake imecheza vizuri na kufungwa ni sehemu ya mchezo.

Stewart alisema haikuwa bahati kwao kwa kuwa walipata nafasi nyingi za wazi umaliziaji ukawa tatizo, pia na penati mbili walizopata wachezaji wake walikosa na kuipa ushindi timu hiyo ilikuwa na mashabiki wengi uwanjani hapo.

“Timu inayocheza vizuri ni ile inayotengeneza nafasi na kucheza mpira mzuri, tulicheza vizuri nafurahi kuona wachezaji wanajituma, kukosa penati na nafasi za wazi ni matatizo yanaweza kuzibika” alisema Stewart

Aliongeza kuwa kupitia mechi hizi zote watakuwa na wakati mzuri wa kurekebisha makosa yanayotokea kabla ya kuanza kwa mechi za ligi.
Katika mchezo huo AFC walikuwa wa kwanza kupata magoli yalifungwa katika dk ya 14 na Paul Were na dk 54 Mike Baraza aliifungia timu hiyo goli la pili kufuatia kosa la beki wa Azam FC, David Mwantika kumruhusu akapiga shuti likaenda moja kwa moja wavuni.

Azam FC walipata penati tatu katika dk 19, Jockins Atudo alikosa baada ya kupiga mkwaju uliotoka nje, dk 65 Khamis Mcha nae alikosa penati baada ya kugonga mwamba na kurudi ndani ikaokolewa na mabeki wa AFC.
Goli la Azam FC lilipatikana kupitia kwa mkwaju wa penati iliyopigwa na Samih Haji Nuhu baada ya beki wa AFC Erick Masika kumwangusha Humprey Mieno kwenye eneo la hatari.

Kipindi cha pili Kocha Stewart alifanya mabadiliko walitoka, Luckson Kakolaki, Salum Abubakar, Abdulhalim Humud, Uhuru Seleman, Jabir Aziz na Gaudence Mwaikimba nafasi zao zikachukuliwa na David Mwantika, Michael Bolou,Humphrey Mieno, Ibrahim Mwaipopo, Brian Umony na Abdi Kassim, mabadiliko hayo yaliimarisha kikosi hicho muda wote wa mchezo.

Baada ya mchezo huo kocha wa AFC, Tom Olaba alisema kupata ushindi kwa kuifunga timu bora ni mafanikio kwake na kuonyesha ukomavu kwa wachezaji wake.
“Unajua Azam FC ni timu nzuri, tulijiandaa na kupanga kikosi ambacho kitapambana na timu hiyo, nimefurahishwa na ushindi huo kwa kuwa nina wachezaji wapya saba katika timu yangu na wamecheza vizuri na kushinda” alisema Olaba.

Azam FC leo Jumapili jioni itacheza mechi ya pili dhidi ya SOFAPAKA kwenye Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, kesho itapumzika na kufanya mazoezi katika Uwanja wa City kabla ya kucheza na KCB katika Uwanja huo siku ya Jumanne.

Azam FC Mwadini Ally, Himid Mao, Samih Haji Nuhu, Luckson Kakolaki/David Mwantika 45’, Jockins Atudo, Jabir Aziz/Humphrey Mieno 45’, Salum Abubakar/Ibrahim Mwaipopo 45’, Abdulhalim Humud/Michael Bolou 45’, Uhuru Seleman/Brain Umony 45’, Gaudence Mwaikimba/Abdi Kassim 60’ na Khamis Mcha.


AFC Leopards Martin Musaliya, Edwin Mafula, Noah Abichi, Erick Masika, Antony Kimani, Martin Imbalambala/Michael Wendera, Benard Mangoli/Benard Ongoma, Patilah Omoto, Victor Ochieng/Edward Seda, Mike Baraza/Noah Wafule na Paul Were

No comments:

Post a Comment